Return   Facebook

The Universal House of Justice

Ridván 2023

To the Bahá’ís of the World

Dearly loved Friends,

Tunahisi furaha kubwa mno kuwa tunaongea na jumuiya ambayo msimamo na azma yake ya juu hustahili wito wake mkuu. Ni mkubwa kiasi gani, ni mkubwa sana kiasi gani upendo wetu kwenu, na jinsi gani roho zetu zinavyopaa kadiri tunavyoona jitihada zenu za dhati na kujitoa kuishi maisha yanayobumbwa na Mafundisho ya Bahá’u’lláh na kutoa maji yatiayo uzima ya Ufunuo Wake kwa ulimwengu ambao una kiu sana. Hisia yenu kali ya kusudi inaonekana wazi. Upanuzi na uimarishaji, shughuli za kijamii, na ushiriki katika mijadala ya kijamii vinaendelea kwa kasi, na upatano wa kiasili wa shughuli hizi kwenye ngazi ya klasta daima unazidi kuonekana dhahiri. Hakuna popote ambapo hili huonekana wazi zaidi kuliko katika maeneo ambako idadi ziongezekazo zinaanza kujihusisha katika safu za jitihada, kila moja ikiwa njia ya kuachilia nguvu ya Imani ya ujengaji jamii.

Katika miezi kumi na mbili iliyomalizika tangu kuanza kwa Mpango wa Miaka Tisa, tumefurahishwa kuona jinsi shughuli hii ya kiroho ya ulimwengu ilivyowavuvia na kuwaamsha marafiki na kuwapa msukumo kwenye maeneo mahsusi ya utendaji. Hatua ya haraka ya kumakinikia imekuwa ni kuweka katika vitendo mipango ambayo huhakikisha kwamba, katika kila nchi na kanda, huibuka angalau klasta moja ambapo hatua ya tatu ya ukuaji imevukwa: mahali ambako idadi kubwa ya watu hufanya kazi kwa pamoja na huchangia kwenye maisha ya jumuiya hai. Wakitambua, hata hivyo, kwamba lengo kwa kipindi hiki cha miaka ishirini na tano ni kuanzisha program ya ukuaji shadidi katika kila klasta ulimwenguni, waumini pia wamejiandaa juu ya ufunguaji wa klasta mpya kwa Imani hali kadhalika kushadididsha juhudi zao katika maeneo ambayo tayari yana program ya ukuaji. Kuna utambuzi uliokuzwa wa fursa kwa ajili ya watangulizi kuinuka katika sehemu zote za ulimwengu—roho nyingi zilizojitoa zinafikiria jinsi zinavyoweza kuitikia fursa hii, na zingine nyingi tayari zimeshafanya hivyo, hili linaonekana dhahiri zaidi kwenye uwanja wa nyumbani lakini zaidi katika uwanja wa kimataifa vile vile. Hii ni mojawapo ya njia kadhaa ambamo, kama tulivyotumaini, moyo wa kusaidiana unadhihirishwa na marafiki kila mahali. Jumuiya ambako nguvu imejengwa zimejidhatiti zenyewe kusaidia maendeleo yanayofanywa katika eneo tofauti—katika klasta, kanda, nchi au hata bara lingine— na njia za kiubunifu zimepatikana ili kutoa hamasa kutokea mbali na kuwezesha tajiriba kushirikishwa moja kwa moja. Wakati huo huo, mbinu ya kimsingi ya kutwaa kile wanachojifunza katika klasta, ili kwamba kiweze kufahamisha mipango inayofanywa ndani na kwingineko, inatumika kwa mapana. Tumependezwa kuona kwamba umakini mahsusi unatolewa kwenye ujifunzaji wa jinsi ya kukuza ubora wa tajiriba ya kielimu itolewayo na taasisi. Wakati mchakato wa taasisi ukiota mizizi katika jumuiya, matokeo yake ni ya kuvutia. shuhudieni, mathalani, vile vituo vya shughuli shadidi ambako wakazi wamekuja kuichukulia taasisi ya mafunzo kama chombo chenye nguvu ambacho ni chao: chombo ambacho maendeleo yake thabiti wameyachukulia kama jukumu lao kuu. Wakijua vyema kwamba milango ya Imani daima ipo wazi, waumini wanajifunza jinsi ya kutoa hamasa kwa wale ambao wapo tayari kuingia. Kutembea na roho kama hizo, na kuzisaidia kuvuka kizingiti, ni upendeleo na shangwe maalum; katika kila muktadha wa kiutamaduni, kuna mengi ya kujifunza kuhusu nguvu za wakati huu wenye mvumo wa utambuzi na hisia ya kuwa sehemu yake. Na si hayo tu. Wakati katika klasta nyingi juhudi za kuchangia kwenye mabadiliko ya kijamii zipo katika hatua zake za mwanzoni kabisa, Mabaraza ya Kiroho ya Kitaifa, daima yakisaidiwa kwa ustadi na Washauri, yanapambana kutaka kujifunza zaidi kuhusu jinsi juhudi hizi zinavyoibuka kutoka kwenye mchakato wa ujengaji jumuiya. Majadiliano kuhusiana na usitawi wa kijamii na kimwili wa watu yanaendelezwa ndani ya makundi ya familia na katika jumuiya, wakati marafiki pia wanatafuta njia kushiriki katika mijadala ya maana ambayo inakunjuka katika mazingira yanayowazunguka.

Katikati ya yote tuliyoelezea, matendo ya vijana hung’aa kwa wangavu. Mbali na kuwa washarabu baridi wa ushawishi—uwe ushawishi unaofaa au vinginevyo— wamejithibitisha wenyewe kuwa washiriki jasiri na maizi wa Mpango. Pale ambapo jumuiya imewaona katika mtazamo huu na kutengeneza mazingira kwa ajili ya maendeleo yao, vijana wamethibitisha zaidi ya imani iliyooneshwa kwao. Wanafundisha Imani kwa marafiki zao na kuifanya huduma kuwa msingi wa urafiki wenye maana zaidi. Mara nyingi—huduma kama hiyo huchukua sura ya kuwaelimisha wale wadogo zao yao—wakiwapatia, siyo tu elimu ya kimaadili na kiroho, bali aghalabu msaada kwa masuala yao ya shule vile vile. Wakiwa na jukumu takatifu la kuimarisha mchakato wa taasisi vijana wa Kibahá’í wanatimiza matumaini yetu pendwa.

Mandhari ya juhudi zote hizi ni zama zilizovurugika sana. Kuna utambuzi ulioenea pote kwamba miundo ya sasa ya jamii inaandaliwa kwa hila kushughulikia mahitaji ya jamii ya binadamu katika taabu zake za sasa. Mengi ambayo yalidhaniwa kwa kiasi kikubwa kuwa ni ya uhakika na yasiyotetereka yanahojiwa, na matokeo ya mkoroganyo huo yanaleta shauku kwa ajili ya muono uunganishao. Kibwagizo cha sauti zilizopaazwa katika kuunga mkono umoja, usawa, na haki huonesha jinsi gani walio wengi hushiriki matamanio haya kwa ajili ya jamii zao. Bila shaka, haishangazi kwa muumini wa Uzuri Uliobarikiwa kwamba mioyo sharti itamani mambo ya kiroho yaliyo mema Aliyoyatoa. Lakini hata hivyo tunaona inavutia kwamba, ndani ya mwaka mmoja wakati matarajio kwa ajili ya maendeleo ya pamoja ya jamii ya binadamu mara chache yameonekana yenye ghamu; mwanga wa Imani uling’aa kwa wangavu wa kustaajabisha katika makongamano zaidi ya elfu kumi, yaliyohudhuriwa na takribani watu milioni moja na nusu, yakimakinikia juu ya njia za kuendeleza mambo hayo hayo mema. Muono wa Bahá’u’lláh, na rai Yake kwa jamii ya binadamu kufanya kazi kwa umoja kwa ajili ya uboreshaji wa ulimwengu ulikuwa ni kiini ambacho kwacho mambo anuwai ya jamii uliyakusanya kwa shauku—na haishangazi, kwani kama ‘Abdu’l-Bahá alivyoelezea, “Kila jumuiya ulimwenguni hupata katika Mafundisho haya Matakatifu utambuzi wa matamanio yake ya juu kabisa.” Baadhi ya watakia heri wa jamii ya binadamu mwanzoni wanaweza kuvutiwa kwenye jumuiya ya Kibahá’í kama mahali pa kimbilio, hifadhi kutoka ulimwengu uliogawanyika na kupooza. Bado, mbali na hifadhi, wanachokikuta ni roho ndugu zikifanya kazi kwa pamoja kuujenga upya ulimwengu.

Mengi yanaweza kuandikwa kuhusu ueneaji wa kijiografia wa makongamano haya, msukumo huu usio wa kawaida yaliyouingiza kwenye Mpango mpya, au sura za dhati za furaha na shauku yaliyoleta kutoka kwa wale waliohudhuria. Lakini katika mistari hii michache tunapenda kuelekeza kwenye kile yalichoashiria kuhusiana na maendeleo ya Hoja. Yalikuwa ni tafakari ya jumuiya ya Kibahá’í ambayo huona undugu, siyo tofauti. Muonekano huu ulifanya iwe kawaida kuchunguza Mpango wa Miaka Tisa kwenye mikusanyiko ambayo kwayo wote walikaribishwa. Marafiki walifikiria matokeo ya Mpango kwa ajili ya jamii zao siyo tu katika mwambatano wa watu binafsi na familia, bali viongozi wa maeneo na wenye mamlaka kadhalika. Kuwaleta pamoja watu wengi hivyo sehemu moja kulitengeza mazingira kwa ajili ya mazungumzo yabadilishayo kuhusu maendeleo ya kiroho na kijamii, yale yanayoukunjua ulimwengu mzima. Mchango maalum ambao mikusanyiko kama hiyo—iliyokuwa wazi, ya kutia moyo, na yenye kusudi—waweza kutoa kwenye ruwaza ipanukayo ya maendeleo ya jumuiya katika klasta ni somo la thamani sana kwa asasi za Kibahá’í kulizingatia kwa siku zijazo.

Na hivyo kundi la waaminifu linaingia mwaka wa pili wa Mpango likiwa na mtazamo mpya na umaizi wa kina kwenye umuhimu wa kile linachotaka kukitimiza. Jinsi gani matendo mbalimbali huonekana yanapotazamwa kwa mtazamo wa nguvu ya ujengaji jamii yanayoiachilia! Matarajio haya yapanukayo huruhusu shughuli inayodumishwa kuonekana kama zaidi ya kitendo kilichotengwa cha huduma au kama mahali tu pa taarifa. Katika kila mahali, jitihada zinazofanyika hufunua ujifunzaji wa watu juu ya namna ya kubeba majukumu yaongezekayo kwa ajili ya kuongoza njia ya maendeleo yake yenyewe. Matokeo ya mabadiliko ya kiroho na kijamii hujidhihirisha yenyewe katika maisha ya watu kwa namna mbalimbali. Katika mfululizo uliopita wa Mipango, ingeweza kuonekana dhahiri kabisa katika uendelezaji wa elimu ya kiroho na ibada ya pamoja. Katika mfululizo huu mpya wa Mipango, umakinifu uongezekao huhitaji kutolewa kwa michakato mingine ambayo hutaka kuinua maisha ya jumuiya—kwa mfano, kwa kuboresha afya ya jamii, kutunza mazingira au kutumia kwa ufanisi zaidi nguvu ya sanaa. Kile kinachohitajika kwa ajili ya pande zote hizi zinazoshamirishana za usitawi wa jumuiya kusonga mbele, bila shaka, ni uwezo wa kujihusisha katika ujifunzaji wenye mpangilio katika maeneo yote haya—uwezo ambao huchota kwenye umaizi unaoibuka kutokana na Mafundisho na hifadhi iliyokusanywa ya maarifa ya mwanadamu yaliyopatikana kupitia udadisi wa kisayansi. Kadiri uwezo huu ukuavyo, mengi yatatimizwa katika miongo ijayo.

Muono huu uliopanuliwa wa ujengaji jamii, una matokeo yanayofika mbali. Kila jumuiya ipo kwenye njia yake yenyewe kuelekea utambuzi wake. Lakini maendeleo katika sehemu moja yana sura zinazofanana na maendeleo katika sehemu nyingine. Sura moja ni kwamba, kadiri uwezo uongezekavyo na nguvu ya jumuiya ya mahali au kitaifa ziongezekavyo, basi, muda ukitimia, vigezo vihitajikavyo kwa ajili ya uibukaji wa Mashriqu’l-Adhkár, vilivyotajwa katika ujumbe wetu wa Riḍván 2012, hatimaye vitatimizwa. Kama tulivyoonesha katika ujumbe wetu kwenu Riḍván iliyopita, kila baada ya kipindi fulani tutabainisha maeneo ambako Hekalu la Kibahá’í litatakiwa kuinuliwa. Tunayo furaha kubwa kuagiza kwa wakati huu, usimikwaji wa Nyumba za Ibada za mahali huko Kanchanpur, Nepal, na Mwinilunga, Zambia. Zaidi ya hili, tunaagiza Nyumba ya Ibada ya kitaifa iinuliwe huko Canada, karibu karibu na Ḥazíratu’l-Quds ya Kitaifa iliyoanzishwa muda mrefu huko Toronto. Miradi hii, na mingine itakayoanzishwa hapo baadaye, itanufaika na msaada unaotolewa kwa ajili ya Mfuko wa Mahekalu kutoka kwa marafiki katika kila nchi.

Ni tele baraka ambazo Bwana mkarimu amechagua kuwajalia wapendwa Wake. Ni mtukufu wito, ni makubwa mno matarajio. Ni zenye uhitaji mno nyakati ambamo sote tumeitwa kuhudumu. Ni zenye hamasa, hivyo, sala ambazo kwazo, kwa niaba yenu na kwa juhudi zenu zisizochoka, tunasali kwenye Kizingiti cha Bahá’u’lláh.

 

Windows / Mac